WANANCHI wa visiwa vya Unguja na Pemba wametakiwa kuhakikisha wanadai risiti wanapofanya manunuzi kwani kutofanya hivyo ni makosa kwa mujibu wa sheria za usimamizi na ukusanyaji wa mapato nchini.

Hayo yalielezwa na Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Amour Hamil Bakar, wakati akizindua kampeni ya siku 14 ya kutoa elimu ya kodi pamoja na kuhamasisha wananchi kudai risiti na wafanyabiashara kutoa risiti wakati wa kununua na kuuza bidhaa katika maeneo ya kituo cha zamani cha daladala Darajani.

Alisema, ikiwa wafanyabiashara watatoa risiti na wananchi kudai risiti basi watakuwa wanatekeleza wajibu wa kisheria wa za kodi katika mauziano hayo.

Aidha alisema ni jambo la msingi kwa wananchi kudai risiti kwani wao ndio walipakodi na pale wanapoopuuza watambue kuwa kodi zao wanaawachia wafanyabiashara na hazifiki serikalini hali ambayo inasababisha mapato mengi kupotea na huduma za kijamii kuzorota.. 

Kamisha Hamil, alibainisha kuwa, dhamira ya uzinduzi wa kampeni hiyo kwa mikoa yote ya Unguja na Pemba ni kuhamasisha wananchi juu ya suala zima la kudai risiti wanapofanya manunuzi yao kwa bidhaa na huduma kutoka kwa wauzaji huku wafanyabiashara kuhakikisha kwamba wanatoa risiti pale wanapofanya mauzo ili kodi hizo ziweze kutumika katika mambo ya kimaendeleo.

Hata hivyo, alisema kampeni hiyo ni muendelezo wa vitendo kutokana na agizo lilotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein, katika baraza la Iddi kuzitaka tasisi zinazosimamia kodi ikiwemo bodi yao na TRA kuhakikisha wanafikisha elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kudai risiti na wafanyabiashara kutoa risiti.

"Katika kutekeleza kwa vitendo agizo lake lile tumeona ni vyema kuja hapa Darajani ambapo ni eneo kubwa linalozungukwa na wafanyabiashara na watu wengi huja kwa ajili ya kufanya manunuzi kuwaelisha juu ya umuhimu wa kudai risiti,"alisema.

Hivyo, aliwaomba wananchi wanaofanya manunuzi kuhakikisha wanadai risiti huku akiwasisitiza wafanyabiashara kutoa risiti ili kuhakikisha mapato ya serikali yanapatikana na hayapotei kiholela.

Safia Ishak ni Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano ZRB, alisema kwa mujibu wa sheria hakuna kiwango kilichowekwa kwa mnunuzi kupatiwa risiti na kuhakikisha anaponunua kitu chochote lazima kupatiwa risiti yake.

Alisema, zamani sheria iliweka ukomo wa shilingi 1000 lakini hivi sasa sheria haina ukomo huo na kwamba ni lazima mwananchi kufahamu kuwa anachonunua chochote anatakiwa kudai risiti.

Sambamba na hayo, aliwasisitiza wafanyabiashara kuwa na maeneo maalum ya kufanyia biashara ili kuweza kujisajili na kuwasisitiza wafanyabishara wakubwa kuhakikisha wanajisajili na wanalipa kodi kwa maendeleo ya nchi yao.

Nao, baadhi ya wananchi waliofika katika maeneo hayo walisema awali walikuwa hawajui umuhimu wa kudai risiti lakini baada ya kupata elimu hiyo wameweza kufahamu umuhimu wa risiti.

Aidha, walisema kitendo cha kudai risiti pia kitawaepusha kuuziwa vitu visivyokuwa vya halali kwani mara nyingi wamekuwa wakiuziwa vitu ambavyo havina ubora na pale wanapovirejesha huwa wanakosa kisibitisho na mfanyabiashara kukataa kumrejeshea pesa zake.

"Kwa kweli elimu hii imetukomboa sana sisi wananchi tunaofanya manunuzi kwani mara nyingi tumekuwa tukiuziwa vitu visivyo vya halali lakini hivi sasa tukiweza kununua bishaa na kupewa risiti basi tutakuwa tumenunua kitu cha halali na pale kitakapokuwa kipovu tunajua pakukimbilia,"walisema.

Hamad Juma, alisema mara nyingi wafanyabiashara wamekuwa wakiuza bidhaa zilizopitwa na muda na wananchi hawana muamko wa kudai risiti hivyo, elimu hiyo imewawezesha kuwafumbua macho na kuhakikisha pale wanapofanya manunuzi hata ya bidhaa ndogo kudai risiti kama wanapofanya wafanyabiashara wa gari, baskeli na bidhaa nyengine za bei kubwa.      

Nae, Mfanyabiashara Suleiman Abdala Saleh, alisema awali walikuwa hawana muamko wa kutoa risiti lakini hivi sasa watahakikisha wanapofanya manunuzi wanatoa risiti kwa ajili ya kuimarisha maendeleo ya nchi yao.

Kampeni hiyo ya siku 14 ambayo imeanzia kwa Mkoa wa Mjini Magharibi na Mkoa wa Kaskazini Unguja na badae kumalizia mikoa mengine ya Zanzibar lengo ni kuona elimu ya ulipaji wa kodi inafika katika maeneo yote.