SHIRIKA la Serikali nchini Singapore linahusika na Mashirikiano (Singapore Cooperation Enterprise) limeingia mkataba na Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ili kuleta ufanisi kwa wafanyakazi wao katika kutanua wigo wa ukusanyaji wa mapato.

Akizungumza katika hafla hiyo, iliyofanyika ofisini kwao Mazizini, Kamishna wa ZRB, Amour Hamil Bakari, alisema malengo ya mkataba huo ni kufanya mabadiliko katika utendaji wa kazi kwa wafanyakazi katika nyanja mbalimbali ikiwemo ukusanyaji bora wa kodi, utandawazi wa kutumia Teknolojia ya ICT.

 Alisema utiaji saini huo ni muendelezo wa makubaliano ambayo yaliwahi kufanyika mwaka 2013 baina ya serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Shirika hilo ili kuweza kufaidika hatua iliyofikiwa ya maendeleo hasa katika eneo la ukushanyaji wa mapato.

“Tumeona ni vyema tutiliane saini makubaliano maalum ambayo yatalenga katika malengo manne (4) ikiwemo kuwajengea uwezo wafanyakazi wetu, kuangalia mifumo yetya  ukusanyaji wa kodi ya VAT, kuangalia suala zima la Teknologia ya habari ya ICT pamoja na masuala mazima ya shughuli za ukusanyaji wa kodi pamoja na mapato mengine ya Serikali”, alisema.

Kamishna Hamil, alibainisha kuwa mabadiliko yapo kabla ya utiaji saini kwani ZRB kuna maeneo ambayo wameshaanza kubadilishana utaalamu na kushauriwa katika masuala ya teknoligia ya habari na suala la ukusanyaji wa mapato.

“Mabadiliko ya kwanza yaliyopatikana kutoka Shirika hili kwa ZRB ni kubadilisha utendaji wa wafanyakazi wetu ambao wanafanya kazi kwa uadilifu wa hali ya juu na kujituma kwa kuhakikisha inaekeleza jambo la msingi la ukusanyaji wa mapato na faida yake tumeiona tumepiga hatua”, alisema.

Katika hatua nyengine alisema madabiliko hayo pia yatakwenda nje ya ZRB hususan kwa walipa kodi wao ambao wanahitaji kufanya nao kazi kwa karibu ili kuhakikisha bodi inakusanya kodi na wao wanaipeleka kodi ya serikali ili kuongeza mapato na kodi hiyo iweze kuendeleza mahitaji mbalimbali ya serikali kwa wananchi wake.  

Hata hivyo, alisema hivi sasa ZRB imefungua ukurasa mpya wa shughuli nzima za utendaji kazi wa ambao utaleta tija kwa Bodi hiyo na Serikali kwa ujumla.

Mbali na hayo, alisema shirika hilo litamteuwa mtaalam anaehusiana na masuala ya ICT pamoja na ukusanyaji wa kodi ambae atakuwa ZRB kwa muda maalum kwa ajili ya kubadilishana ujuzi na kuona lengo la ukusanyaji wa mapato linafikiwa kama ilivyokusudiwa.

 Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Singapore Coperetion Enterprise kuhusu masuala ya Afrika Bi. Neo Pol Ling, alisema ushirkiano huo utakuwa mzuri na kuleta mabadiliko kwa wafanyakazi katika utendaji wao wa kazi na ukusanyaji wa kodi katika kuongeza pato la taifa.

Alisema, lengo lao ni kutoa misaada ya kiutendaji ili kufikia kasi ya maendeleo kama iliyofikia nchi yao.

  • Viongozi wa Bodi Ya Mapato Zanzibar (ZRB) wakiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Singapore Cooperation Enterprise (SCE) mara baada kutia saini Hati za Makubaliano baina ya ZRB na SCE
  • Viongozi wa Bodi Ya Mapato Zanzibar (ZRB) wakiwa katika picha ya pamoja na Wawakilishi wa Singapore Cooperation Enterprise (SCE) mara baada kutia saini Hati za Makubaliano baina ya ZRB na SCE