BODI ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) imewatoa hofu wawekezaji nchini kuwa imejidhatiti kuhakikisha wanawaondolea changamoto wanazokabiliana nazo katika ulipaji kodi ili kuwarahisishia ufanyaji wa biashara zao

Hayo yalielezwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Saleh Sadiq, wakati akizungumza waandishi wa habari katika Hoteli ya Melia iliyopo Kiwengwa mara baada Bodi hiyo ya Wakurugenzi kumaliza ziara ya kuwatembelea baadhi ya wawekezaji nchini kwa lengo la kufahamu namna miradi yao inavyoendeshwa.

Alisema, kuna changamoto nyingi wamezibaini katika ziara hiyo lakini serikali itahakikisha kila mfanyabiashara na mwananchi anapata haki yake na kuwapa unafuu ili kuona biashara zao zinakwenda kama iliyokusudiwa na zinatoa tija inayotakiwa.

“Serikali siku zote ipo pamoja na wawekezaji, tunawatoa hofu, changamoto munazokabiliana nazo tupatieni, na tutazifikisha Serikali ili kuangalia namna ya kuzipatia ufumbuzi”, alisema

Aidha, alisema moja changamoto kubwa walizozibaini ni wafanyabiashara wa Zanzibar kulipishwa kodi mara mbili pindi wakifanya biashara baina ya Zanzibar na Tanzania bara hivyo watahakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi kwa kupeleka warka Serikalini ili kuona wafayabiashara wanapata afueni katika kulipa kodi.

Mwenyekiti Sadiq, alibainisha kuwa, pia Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na Makamo wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania wanakaa na kutafuta suluhu ya kulitatua changamoto kaza zikiwemo hizi za kodi baina ya pande mbili za Muungano (Zanzibar na Tanzania Bara).

Alisema, lengo la serikali kukakiribisha wawekezaji ni kukuza uchumi wa nchi na kuongeza mapato kwa kuhakikisha viwanda vya Zanzibar vinaimarika na kupata kodi Stahiki na kwa wakati.

Hata hivyo, alisema ZRB itahakikisha inafanya kazi kwa makini ili kuona kiwango cha ukusanyaji wa kodi kilichokadiriwa na serikali kwa mwaka 2017/2018 kinafikiwa kama ilivyokusudiwa.

Hivyo, aliwasisitiza walipa kodi kuacha tabia ya kufanya uvivu katika kulipa kodi na badala yake walipe kodi ili serikali iweze kufanikisha shughuli zake za kuwapatia maendeleo wananchi.

“Ni vyema walipa kodi kuacha tabia ya kukaa muda mrefu kulimbikiza madeni kwani ZRB ni tasisi pekee inayoisaidia serikali katika ukusanyaji wa mapato ambayo yanatumiwa kwa huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, miundombinu ya maji safi na miundombinu mengine muhimu,” alisema.     

Mkuu wa Kitengo cha Utawala kiwanda cha Maji Drop of Zanzibar, Mahmoud Hussein, alisema pamoja na bidhaa yao kuwa na ubora lakini mahoteli mengi huwa hawanunui maji yanayozalishwa Zanzibar na badala yake kununua yanayotoka Tanzania  bara jambo ambalo linapelekea kushuka kwa soko lao.

Changamoto nyengine, alisema ni umeme kuzimwa mara kwa mara bila ya taarifa hali ambayo inasababisha kuharibika kwa mashine zao na kusababisha hasara kubwa kwa kiwanda.

Hivyo, aliiomba bodi hiyo kuwatatulia changamoto hizo ili kuona wanapata kipato na kulipa kodi kwa wakati kama inavyotakiwa.

BODI ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) ilifanya ziara ya kutembelea hoteli ya Verde Zanzibar Azam Luxary resort and Spa Limited iliyokuwepo Maruhubi, Kiwanda cha Maji ya Drop kilichopo Hanyegwa Mchana na Melia Zanzibar Hotel iliyopo Kiwengwa.

  • Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) wakimsikiliza Msaidizi meneja wa Verde Hotel iliyopo MtoniWajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) wakimsikiliza Msaidizi meneja wa Verde Hotel iliyopo Mtoni