BODI ya Mapato Zanzibar (ZRB) imetoa msaada wa vifaa vya skuli kwa watoto yatima wanaolelewa katika nyumba ya Mazizini ikiwa ni shamrashamra za miaka 55 ya Mapinduzi ya Zanzibar na shamrashara za kutimiza miaka 20 ya kuanzishwa kwa bodi hiyo.

Vifaa vilivyotolewa kwa watoto hao ni pamoja na mikoba ya skuli na vifaa kamili vya kusomea ikiwemo mabuku, peni penseli raba, kichongeo mstari, kampas na kava.

Akizungumza na watoto hao kwa niaba ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Saleh Sadiq, Meneja Kitengo cha Mahusiano na Huduma kwa Walipakodi ndugu Shaaban Ramadhan Yahya, alisema msaada huo ni moja ya kuunga mkono jitihada za Dk. Shein katika kuiendeleza sekta ya elimu nchini.

Shaaban, alisema ZRB kama wadau wa maendeleo Zanzibar inaunga mkono dhana nzima iliyotolewa na Dk. Shein hivi karibuni wakati akifungua skuli kisiwani Pemba ya kuhakikisha wanafunzi wanasoma bure na hawachangishwi hata ufagio. 

“ZRB tumefika katika nyumba hii ili kutimiza malengo ya Rais wetu wa Zanzibar Dk. Ali Mohammed Shein ya kutoa elimu bila ya malipo,” alisema.

Hata hivyo, alibainisha kuwa, serikali imekuwa ikitoa mambo mbalimbali katika sekta ya elimu nchini ikiwemo majengo na vifaa lakini kuna mambo mengine ambayo hayatoshelezi na  lazima wadau wengine wanahitaji kuchangia ili kuhakikisha watoto wanasoma katika mazingira mazuri.

Sambamba na hayo alibainisha kuwa ZRB itaendelea kutekeleza ahadi yake ya kupeleka vitambaa vya sare za skuli na magodoro katika kituo hicho ili watoto hao nao waweze kuvaa sare mpya katika mwaka wa masomo.

Alitumia muda huo kuziomba tasisi nyengine na watu binafsi kuunga mkono jitihada za serikali na kuona kuna watoto ambao wanahitaji malezi yao na viogozi bora watakaochangia katika maendeleo ya nchi yao.

Nae, Mdhamini wa kituo hicho, Chumu Ali Abeid, aliipongeza bodi hiyo kwa msaada walioutoa kwa watoto hao na kuwaomba usiwe mwisho na kuendelea kuwasaidia kwani watoto hao wanamahitaji mengi ambayo wanahitaji kusaidiwa.

Mmoja wa wanafunzi hao Rukia Ali Daudi akitoa shukrani kwa niaba ya watoto wenzake aliiupongeza uongozi wa ZRB kuwapa msaada huo na kuahidi kusoma kwa bidii.

Pia alitumia muda huo kumpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohammed Shein  kuwajali watoto waliokuwepo katika kituo hicho na kuwajengea mazingira mazuri nao kujiona kama watoto wengine wenye familia zao.

Jumla ya wanafunzi 29 wa kidato cha tano, kidato cha pili, darasa la sita, darasa la kwanza, lapili na maandalizi wanaolelewa katika kituo hicho wamepatiwa msaada huo ambao umegharimu zaidi ya milioni tatu. 

  • Maafisa wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) wakishiriki katika utoaji wa vifaa vya Skuli Kwa watoto wanaolelewa katika Kituo cha kulelea Watoto Yatima Mazizini Zanzibar.Maafisa wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) wakishiriki katika utoaji wa vifaa vya Skuli Kwa watoto wanaolelewa katika Kituo cha kulelea Watoto Yatima Mazizini Zanzibar.