KAMISHNA wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), Joseph Abdalla Meza, amewasisitiza wafanyabiashara kuhakikisha wanafuata masharti ya biashara ikiwemo kulipa kodi kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar.

Alieleza hayo wakati akizungumza na wafanyabiashara wakubwa wanaoingiza bidhaa nchini katika kikao kilichoandaliwa na kamati ya usimamizi ya Bodi ya Wakurugenzi ya ZRB chenye lengo la kuzungumza na wafanyabiashara hao kujua changamoto zao ili ziweze kufanyiwa kazi.

Alisema, ikiwa wafanyabiashara watafanya vile ambavyo sheria inavyosema basi wataweza kuijenga nchi yao na kuziwezesha biashara zao kwenda vizuri. 

Aidha, alisema wafanyabiashara wanapaswa kulipa kodi kwa viwango vilivyowekwa na serikali na kuongeza uwajibikaji katika ulipaji wa kodi nchini.

Alibainisha kuwa, serikali nyingi duniani zinaendeshwa kwa kodi sambamba na kuwa na mashirikiano baina yao na tasisi za ukusanyaji wa kodi.

Kamishna huyo, alifahamisha kuwa, ni jambo la msingi kwa wafanyabiashara kufahamu kuwa nchi ya Zanzibar inajengwa na wanazalendo wenyewe hivyo ni vyema kuzingatia suala la ulipaji wa kodi.

Sambamba na hayo, alisema serikali imekuwa ikijitihadi kuweka mazingira mazuri katika maeneo mbalimbali ili kuhakikisha biashara zao zinakwenda vizuri hivyo kama hawatochangia mambo hayo hayawezi kufikiwa.

“Ni vyema nyinyi wafanyabiashara kuwa wakweli katika kulipa kodi kwani wananchi wanaitegemea sana Serikali katika mambo muhimu ya kimaendeleo ikiwemo Afya, elimu, miundombinu ya maji, barabara na miundombinu nyengine kama nyinyi hamtoweza kulipa kodi na kufanya udanganyifu basi wananchi wataendelea kutoiamini Serikali yao waoneeni huruma kwani wao ni walipa kodi na sote kwa pamoja tuhakikishe tunakuza uchumi wa nchi yetu,” alisisitiza.

Akizungumzia changamoto ya ufinyu wa bandari unaolalamikiwa na wafanyabiashara unaosababisha msongamano wa makontena, alisema Serikali ina mpango wa kujenga bandari mpya ya Mpiga duri ambayo itaweza kuondosha changamoto hiyo.

Katika hatua nyengine, alisema ZRB itaendelea kushirikiana na wafanyabishara ili changamoto zilizopo zinafanyiwa kazi na lengo la ukusanyaji wa mapato linafikiwa.

Mbali na hayo, alitumia muda huo kuwasihi wafanyabishara kuhakikisha wanapofanya biashara wanatoa risiti na wananchi ambao wanafanya manunuzi kudai risiti kwani ni jambo muhimu na lipo kisheria.

Mweyekiti wa Kamati hiyo, Mcha Hassan Mcha, ambae pia ni Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar, aliwahakikishia wafanyabiashara hao kuwa watahakikisha wanakaa pamoja na ZRB na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowahusu.

Nao, wafanyabishara hao waliiomba ZRB kuweka mazingira mazuri ambayo yatamuwezesha mfanyabiashara kuweza kulipa kodi na kuwa chachu ya maendeleo katika kukuza uchumi wa nchi.

Hata hivyo, waliiomba ZRB kuwafatilia wafanyabishara wakubwa ambao wanafanya udanganyifu katika suala la kulipa kodi na kuikosesha Serikali mapato yake.

“Sisi sote ni wazalendo wa nchi hii na lengo letu ni kuona tunalipa kodi kwa manedeleo ya nchi yetu hakuna mfanyabiashara ambae hataki maendeleo,” walisema.