Mamlaka za Mapato EAC Zasisitizwa Mapambano Dhidi ya Rushwa, Uhalifu wa Kifedha
Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Said Kiondo Athumani, wakati akifungua Mkutano wa 21 wa Kamati ya Kiufundi ya Uadilifu ya Mamlaka za Mapato Afrika Mashariki,
Mamlaka za Mapato za Afrika Mashariki zimesisitizwa juu ya umuhimu wa kuimarisha matumizi ya ushahidi wa kitaalamu kwa kutumia Mifumo (forensic evidence) katika mapambano dhidi ya rushwa na uhalifu wa kifedha.
Msisitizo huo umetolewa leo na Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Said Kiondo Athumani, wakati akifungua Mkutano wa 21 wa Kamati ya Kiufundi ya Uadilifu ya Mamlaka za Mapato Afrika Mashariki, katika Hoteli ya Madinat al Bahr, Mbweni nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Alisema dhamira ya pamoja kuimarisha uadilifu ni msingi muhimu si tu wa kuboresha ukusanyaji wa mapato, bali pia wa kulinda uhalali, uaminifu na taswira ya aasisi za umma pamoja na nchi kwa ujumla.
Alibainisha kuwa, matumizi ya ushahidi wa kitaalamu, ikiwemo uchunguzi wa kidijitali, uchambuzi wa taarifa za kifedha na nyaraka mbalimbali, huongeza usahihi na ufanisi wa uchunguzi, hupunguza mianya ya uingiliaji wa ndani na kuongeza imani ya umma kwa taasisi za mapato.
Kiondo aliwahimiza wajumbe wa mkutano huo kushiriki kwa uwazi na uaminifu, kujadili kesi halisi, kubadilishana mbinu za kisasa za uchunguzi, matumizi ya teknolojia ya forensics na mikakati ya kujenga uwezo wa ndani wa uchunguzi katika mamlaka zao.
Naye Mwenyekiti wa kamati hiyo, James Abola, alisema nchi hizo zimekubaliana kuongeza msisitizo katika hatua za kinga kama mkakati mkuu wa kuimarisha uadilifu ndani ya Mamlaka za Mapato na kuendeleza uchunguzi na hatua za kinidhamu dhidi ya wanaokiuka maadili ya utumishi wa umma.
Alibainisha kuwa uchambuzi wa hatari za uadilifu (integrity risk profiling) umetambuliwa kama nyenzo muhimu ya kinga inayopaswa kupewa kipaumbele katika Mamlaka zote za Mapato za Afrika Mashariki.
Kwa upande wake Katibu wa kamati hiyo ambae pia ni Mkurugenzi Idara ya Mambo ya ndani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ndugu Shaibu Mmari, alisema wamejipanga kuwafundisha watumishi wao namna bora ya kutumia vifaa vya forensics kwa ajili ya kukamata na kuhakiki watu wanaotenda makosa na ukiukwaji wa maadili.
Pamoja na hilo alisema moja ya maazimio yao ni kila nchi kwenda kutengeneza kanuni za kimaadili ili kuwa na aina moja ya mfumo wa ukamataji, uhakiki wa taarifa za forensics na njia moja ya kuwasilisha taarifa hizo katika nchi zao.
Mkutano huo wa siku tatu (3) unawashirikisha wajumbe kutoka mamlaka mbalimbali za mapato, zikiwemo Mamlaka ya Mapato Kenya (KRA), Rwanda Revenue Authority (RRA), Burundi Revenue Authority, Somalia Revenue Authority, Mamlaka ya Mapato Uganda, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).
Na Muandishi Wetu.

