Wajumbe wa Kamati ya Uchumi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar wameupongeza Uongozi wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) kwa kufikisha huduma karibu na wananchi kulikotokana na kufungua ofisi katika maeneo mbali mbali ya Zanzibar.

Akitoa pongezi hizo katika ukumbi wa ZRB Mazizini wakati wa majumuisho ya ziara ya kukagua ofisi za mikoa za ZRB, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi ya Baraza la Wawakilishi Mheshimiwa Dr. Soud Nahoda Hassan alisema kitendo cha kufungua ofisi katika maeneo mbali mbali si tu kinawasogezea huduma wananchi bali pia ni chachu ya ongezeko la ukusanyaji wa mapato.

Aidha, Mwenyekiti huyo aliwapongeza watendaji wa ZRB kutokana na ufuatiliaji wao wa karibu kwa walipakodi wasiowajibika kwa wakati ambao pasi na ufuatiliaji huo kunaweza kusababisha hasara kwa taifa kwa kupelekea uvujaji wa mapato.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyotembelea ofisi za ZRB Kiwengwa, Nungwi, Michenzani Mall na Mazizini, mjumbe wa Kamati hiyo Bi. Panya Ali Abdallah aliwataka wananchi wa Mkoa wa Kaskazini kuzitumia ofisi hizo na kulipa kodi kwa wakati kwani Serikali tayari imeshawapunguzia masafa kwa kufungua ofisi katika maneo yao.

Pamoja na hayo, Bi. Panya aliihimiza ZRB kutoa elimu zaidi kwa wananchi wafahamu uwepo wa ofisi hizo pamoja na kuwapa elimu ya faida za kodi ili iwape hamasa ya kuwajibika kwa hiyari.

Naye ndugu Mohamed Shafi kwa niaba ya walipakodi wengine wa Mkoa wa Kaskazini Unguja alitoa pongezi kwa ZRB kwa kuwafungulia ofisi karibu na maneo yao ya biashara, na kutanabahisha kuwa pamoja na kuwapunguzia muda wa kufuata huduma, lakini pia jambo hilo linawapa muda mrefu wa kushughulika na biashara zao badala ya kwenda kupanga foleni ofisi za ZRB mjini kama ilivyokuwa zamani.

***************************************Mwisho*****************************************

JEE WAJUA?

Katika Mkoa wa Kaskazini Unguja, Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) wanazo ofisi zao katika eneo la Kiwengwa na Nungwi. Kwa walipakodi wa Mkoa huo wanaweza kupata huduma zetu katika ofisi hizo.

HABARI IKUFIKIE

Uwasilishaji wa Ritani na malipo ya kodi unafanyika kuanzia tarehe 1 hadi 20 ya kila mwezi, huna haja ya kusubiri tarehe 20 kuwasilisha ritani na malipo, unaweza kuwasilisha tarehe za mwanzo ili kuepuka usumbufu wa kuwasilisha siku za mwisho.

FAHAMU

Asiyetoa Risiti anatenda kosa, na akibainika adhabu yake ni shilingi milioni mbili (2) au Kwenda jela mwaka mmoja.