Na Mwandishi Wetu.

Kamisheni ya Utumishi wa Umma Zanzibar imeikabidhi Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) muundo wa taasisi hiyo kufuatia mabadiliko ya kimuuondo ya kutoka iliyokuwa Bodi ya Mapato Zanzibar yaliyofanyika hivi karibuni.

Akizungumza baada ya kukabidhi Muundo huo Katibu wa Kamisheni ya Utumishi wa Umma ndugu Kubingwa Mashaka Simba aliipongeza ZRA kwa kuja na muundo mpya unaokwenda sambamba na kasi ya Serikali ya awamu ya nane (8).

Katibu Kubingwa alisema muundo huo wenye jumla ya Idara nane (8) na Vitengo sita (6) pamoja na ofisi za Mikoa, unatarajiwa kupunguza gharama za uendeshaji kwa wastani wa milioni 37 kwa mwezi ikilinganishwa na muundo wa awali.

Aidha, Katibu huyo alisema mabadiliko haya ya muundo wa ZRA yamefanyika ili pamoja na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi, bali pia ni kwa lengo la kuendana na miundo ya taasisi nyengine za kikanda za ukusanyaji wa kodi.

Katibu Kubingwa alisisitiza kuwa baada ya makabidhiano ya muundo huo, Mamlaka ya Mapato Zanzibar inapaswa kuanza mara moja matumizi yake ili kukidhi matarajio ya Serikali katika ukusanyaji wa mapato.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa Muundo huo, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar ndugu Yusuph Juma Mwenda alisema ZRA itautekeleza muundo huo zaidi ya matarajio ya Serikali na kuongeza kuwa utaongeza ufanisi katika ukusanyaji wa kodi.

Alifafanua kuwa muundo huo umesadifu muelekeo wa ufanyaji kazi wa taasisi za kodi duniani na kwamba nafasi za uongozi katika muundo huo zitajazwa kwa mfumo wa ushindani kama ilivyoelekezwa na sheria.

Muundo huu mpya wa ZRA pamoja na mambo mengine unatoa nafasi kwa mabadiliko ya vyeo vya taasisi hiyo ambapo sasa Kutakuwa na Kamishna Mkuu, Wakuu wa Idara ambao watakuwa Kamishna, Wakurugenzi, Wakuu wa Vitengo pamoja na Wakuu wa Divisheni.