Na Mwandishi Wetu.

Mamlaka zinazosimamia ukusanyaji wa mapato Zanzibar zimeshauriwa kutafuta chanzo mbadala cha ukusanyaji wa mapato badala ya kuweka mkazo katika kubuni na kuanzisha vyanzo vipya vya kodi.

Rai hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Utawala kutoka Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar ndugu Abubakar Mohamed Abubakar wakati akiwasilisha mada katika Jukwaa la Wadau wa Kodi lililofanyika Katika ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mayugwani.

Mwenyekiti huyo alisema, wakati umefika kwa Mamlaka ya mapato Zanzibar (ZRA) na Mamlaka ya Mapato Tanzania kufanya utafiti ili kuangalia namna nyengine ya kukusanya mapato kwa kuzingatia kuwa wapo wafanyabiashara wengi wamekuwa wazito kulipakodi kulingana na misimamo ya imani zao za dini.

Alifafanua kuwa, kuna kundi kubwa la wafanyabiashara ambao kwa kutumia imani na misimamo ya dini wamekuwa na tabia ya kutowajibika katika kulipa kodi wakiamini kuwa utaratibu wa kulipa kodi ni kinyume na misingi ya dini.

Kwa madhumuni ya kuhakikisha jamii yote na wafanyabiashara wa dini zote wanawajibika katika kuchangia mapato na ukusanyaji wa nchi, ni vyema utafiti ukafanyika ili kuwapa fursa ya kuwajibika kwa hiyari nje ya utaratibu wa kodi.

Akijibu suali la sababu za kufutwa kwa Sheria ya Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) na kuanzishwa kwa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Mwanasheria kutoka ZRA ndugu Khamis Jaffar Mfaume alisema, pamoja na mambo mengine, mabadiliko haya yamelenga kuimarisha huduma kwa walipakodi.

Aidha, Mwanasheria huyo alisema kuwa sababu nyengine za marekebisho hayo ni kuendana na miundo mengine ya taasisi za ukusanyaji mapato za Kikanda.

Jukwaa la Wadau wa Kodi Zanzibar ambalo huwakutanisha viongozi wa ZRA, TRA, Jumuiya za Wafanyabiashara pamoja na wadau mbali mbali limejadili mambo mbali mbali yanayohusu kodi na biashara Zanzibar.