Na Mwandishi Wetu.

Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) inajipanga kuunda timu maalum kwa lengo kukagua mashine na mfumo wa kutolea Risiti za kielektroniki ili kuwabaini wanaokwepa kutoa Risiti kwa kisingizio cha ubovu wa Mashine.

Uamuzi huo ni sehemu ya makubaliano yaliyofikiwa baina ya ZRA na Kampuni zinazouza mashine hizo Zanzibar yaliyotokana na kikao kilichofanyika leo Makao Makuu ya ZRA, Mazizini Zanzibar.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo ndugu Yusuph Juma Mwenda alisema kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara ambao hawatoi Risiti za Kielektroniki wakisingizia ubovu wa Mashine bila ya kufuata utaratibu, jambo ambalo ni kinyume na Sheria.

Ili kuitatua changamoto hiyo, pamoja na changamoto nyengine za uwajibikaji wa katika utoaji wa Risiti, ZRA kwa kushirikiana na Wauzaji wa Mashine za kutolea Risiti inajiandaa kufanya zoezi la pamoja kuwabaini wasiowajibika Unguja na Pemba.

 Akizungumza katika kikao hicho kilichokutana kwa lengo la kujadili changamoto za matumizi ya mashine hizo, Muwakilishi kutoka Kampuni ya Selcom ndugu Geofrey Mwakamyanda alitoa rai kwa Serikali kuweka mikakati imara ya kuwafikia walipakodi ambao bado hawana mashine, jambo litakalosaidia usambazaji wa Mashine na kuongeza utoaji wa Risiti za Kielektroniki.

Ndugu Saleh Salim Saleh kutoka Web Technologies alisema baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakisingizia ubovu wa mashine ili kukwepa kutoa Risiti, na kueleza kuwa kampuni yake ni nadra kupokea taarifa rasmi za kuharibika kwa mashine jambo linatoa taswira kuwa madai ya wafanyabiashara hao si ya kweli.

Pamoja na mambo mengine, kikao hicho kilijadili mambo tofauti yanayohusu usambazaji wa mashine za kutolea Risiti za Kielektroniki pamoja na uharakishwaji wa matengenezo kwa mashine zinazopata hitilafu.

Kikao kilichofanyika leo kujadili changamoto za matumizi ya Mashine za kutolea Risiti za Kielektroniki kimejiri kufuatia ziara ya Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Fedha na Mipango Mheshimiwa Dkt. Saada Mkuya Salum aliyoifanya kwa Wauzaji hao hivi karibuni na kuitaka ZRA kuchukua hatua za haraka za utatuzi wa changamoto .

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa ZRA, pamoja na Kampuni za Pergamon, Web Technologies pamoja na Selcom ambazo ndizo zinauza Mashine za kutolea Risiti za Kielektroniki Zanzibar.