Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imesema inatarajia kuzindua mfumo mpya wa ukusanyaji wa mapato ambao unaendana na mahitaji ya wakati ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato nchini.

Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo ndugu Yusuph Juma Mwenda ameyasema hayo leo huko Maruhubi wakati wa majaribio ya mfumo huo yanayofanywa na watendaji wa ZRA kabla ya kuutangaza rasmi na kuanza kutumiwa na walipakodi.

Kamishna Mkuu Mwenda alisema mfumo huo utakaojuilikana kwa jina la Zanzibar Integrated Domestic Revenue Administration System (ZIDRAS) utawawezesha walipakodi kuwajibika katika majukumu yao kwa njia ya mtandao ikiwemo Kujisajili, kuwasilisha ritani pamoja na kufanya malipo pasi na kufika katika ofisi za ZRA.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa majaribio hayo Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA ZRA ndugu Issac Mohamed alisema mfumo huu unakuja kuchukua nafasi ya mfumo wa Zanzibar Integrated Tax Administration System (ZITAS) ambao kwa sasa ndio unaotumika katika ukusanyaji wa mapato.

Naye Bi. Saada Kassim Khamis ambaye ni Naibu Mkurugenzi anayeshughulikia Walipakodi wa kati na wadogo alisema ni matarajio ya ZRA kuwa ujio wa mfumo huo utaongeza uwajibikaji kwa walipakodi na kuimarisha ukusanyaji wa mapato yanayokusanywa na ZRA.

Aidha, Ndugu Suleiman Mohamed Iddi ambaye ni Meneja katika Idara ya Walipakodi wakubwa ambaye ni mshiriki katika majaribio hayo alisema mfumo huo utakuwa ni msada mkubwa kwa walipakodi anaowasimamia kwa kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakiihimiza ZRA katika kutoa huduma kwa njia ya mtandao.

<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<<MWISHO>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>>

JEE WAJUA?

Wafanyabiashara ambao wanakodisha Nyumba binafsi za kulaza wageni kwa njia ya mtandaokwa njia ya kulaza (Air bnb, Booking .com) wanapaswa kusajiliwa ZRA na kulipa kodi.

 

FAHAMU

Mlipakodi yeyote ambaye amefunga biadhara, au amebadili eneo la biashara au aina ya biashara anapaswa kutoa taarifa kwa maandishi kwa kamishna Mkuu wa ZRA

 

HABARI IKUFIKIE KUWA…

Watoa huduma za kitaalamu wanapaswa kusajiliwa na ZRB katika kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).