Na Muandishi Wetu.

Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) leo imekutana na Wafanyabiashara na Wasafirishaji wa Mwani Zanzibar na kujadili changamoto mbali mbali zinazowakabili kuhusiana na biashara na Kodi katika kikao kilichofanyika Afisi kuu za ZRA Mazizini.

Katika kikao hicho ambacho kiliwahusisha wafanyabiashara pamoja na uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC), kilijadili changamoto kadhaa zinazowakabili wafanyabiashara ya Mwani ikiwemo usajili, aina ya kodi wanayopaswa kulipwa pamoja na mazingira ya biashara ya Mwani Zanzibar.

Akizungumza wakati wa majumuisho ya Kikao hicho Kamishna Mkuu wa ZRA ndugu Yusuph Juma Mwenda alisema ZRA haitaingilia utaratibu wa usafirishaji wa Mwani au bidhaa yoyote kwa mujibu wa sheria wakati changamoto hizi zikiendelea kutafutiwa ufumbuzi. 

Aidha, ZRA imezipokea changamoto zilizowasilishwa na wasafirishaji hao wa Mwani na kuahidi kuzitafutia ufumbuzi ndani ya kipindi cha mwezi mmoja ili kusaidia kupata usuluhishi bora na kuwezesha ustawi wa biashara ya Mwani nchini

Mkurugenzi wa ZRA ofisi ya Pemba aliwahimiza wafanyabiashara hao kuwa wawazi katika biashara zao wanazozifanya ili kuzuia upotevu wa mapato sambamba na kuiwezesha Serikali kuwasaidia katika kuweka sawa mazingira ya biashara.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) ndugu Ali Amour aliwakumbusha wafanyabiashara kukaa na Serikali na kujadili changamoto zinapojitokeza badala ya kugoma kufanya biashara au kusafirisha bidhaa husika.

Kikao hicho cha kujadili changamoto zilizopo katika usafirishaji wa Mwani Zanzibar kilihudhuriwa na Viongozi wa ZRA, Uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Zanzibar (ZNCC) pamoja na Kampuni mbali mbali usafirishaji wa Mwani ikiwemo ZEXA, Zanea Sea Weed, A & Z Export Traders na Zanque Aqua Farms.