BODI ya Mapato Zanzibar (ZRB), imeandaa mpango maalum wa kuanzisha mfumo wa kodi wa vitalu (Block Management System) katika shehia zote za Unguja na Pemba ili kuimarisha ukusanyaji wa mapato nchini.

Mfumo huo utasaidia kujua idadi ya wafanyabiashara waliopo katika shehia, waliosajiliwa kulipa kodi na wanaokwepa kulipa kodi.

Meneja sera na utafiti wa bodi hiyo, Ahmed Saadat Haji, aliyasema hayo wakati akizungumza na masheha wa Wilaya ya Mjini katika ofisi za Mkuu wa Wilaya Amani Unguja.

Alisema, mpango huo utasaidia ukusanyaji mapato kwa bodi hiyo na kupata mapato yake kwa uhakika zaidi kwani mfumo huo umeshaanza kwa majaribio katika shehia ya Nungwi na umeleta mafanikio.

Alisema mfumo huo pia utaendana na Teknolojia kuhakikisha mfanyabishara anaejaza fomu ya maombi ya usajili lazima apitie kwa Sheha na baadae kuingizwa katika mtandao ambao utarahisisha ZRB kutambua idadi ya wafanyabiashara waliopo katika Shehia.

Alisema Sheha ana jukumu kubwa la kutambua wafanyabiashara waliopo katika eneo lake na kama wanalipa kodi.

Alisema jambo la msingi kwa masheha kusimamia kifungu namba tano cha ukusanyaji kodi katika maeneo yao na kuhakikisha kinatekelezwa vyema na wafanyabiashara.

Alisema, nchi haiwezi kujiendesha bila ya kuwa na mapato ya kuaminika, hivyo ipo haja kwa masheha kushirikiana na bodi hiyo katika kufanikisha suala hilo.

Sambamba na hayo, alisema eneo ambalo linaleta changamoto kubwa ni wilaya ya mjini kwani kuna wafanyabiashara wengi wanaofanya udanganyifu kwa kukwepa Kodi.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Mahusiano kwa Umma cha ZRB Safia Is-hak Mzee, alisema kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili Bodi hiyo katika ukusanyaji mapato ikiwemo wafanyabishara kudanganya sehemu wanazofanyia biashara zao hivyo kuja kwa mfumo huo utaonesha sehemu husika anayofanyia biashara yake.

Changamoto nyengine, alisema ni suala la magendo ambalo mara nyingi hujitokeza katika Bandari Bubu, Nyumba zinazolaza wageni bila kusajiliwa na maghala yasiyosajiliwa.

Hivyo, aliwaomba Masheha hao kushirikiana katika kutoa taarifa za mambo hayo pale yanapojitokeza.

Nao Masheha waliopatiwa mafunzo hayo, walisema wamejifunza mambo mengi ambayo yapo katika shehia zao na kuahidi kusimamia vyema kazi hiyo.