Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) imesema kuimarika ukusanyaji wa kodi kutasaidia kukuza huduma mbalimbali za maendeleo nchini. Hayo yalielezwa na Mkuu wa kitengo cha mawasiliano kutoka bodi hiyo, Safia Is-hak, katika mafunzo ya siku moja ya waandishi wa habari, kuhusiana na mabadiliko ya sheria za kodi, yaliyofanyika Mazizini.

Alisema lengo la serikali ni kuinua mapato ya nchi na kuimarisha huduma mbalimbali za maendeleo kwa jamii, hata hivyo, lengo hilo haliwezi kufikiwa kama haitakuwa na fedha za kutosha.

Alisema serikali inahitaji fedha kwa ajili ya kujenga na kuimarisha maeneo tofauti ya kiuchumi na kustawishia maendelo ya wananchi.

Awahimiza wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanalipa kodi kwa wakati na kiwango kinachostahiki.

Nae Mwanasheria wa bodi hiyo, Khamis Jaffar Mfaume, alitumia fursa hiyo kuwaomba waandishi wa habari kutumia nafasi waliyonayo kuwahamasisha wananchi hasa wafanyabiashara kulipa kodi.